HIFADHI ya Taifa ya Serengeti inayopita katika mikoa ya
Arusha,Mwanza,Mara na Shinyanga ni eneo pekee duniani lenye kundi kubwa la
wanyama wanaohama katika mfumo mzima wa mlishano.
Inasemekena neno Serengeti linatokana na neno la kimasai la
sirenget lenye maana ya uwanda mpana wa nyasi fupi,malisho mengi na maji
ya kutosha pengine ndiyo maana hifadhi hiyo inapewa majina mengi kama vile bustani
ya Afrika na Edeni ya Afrika kutokana na utajiri wa maliasili uliopo ndani ya
hifadhi hii.
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti yenye ukubwa wa kilometa za
mraba 14,763 ilianzishwa mwaka 1951, ni Hifadhi ya Taifa ya pili kwa ukubwa
nchini ikitanguliwa na hifadhi ya Taifa ya Ruaha yenye ukubwa wa kilometa za
mraba 20,226.
Umaarufu wa hifadhi ya Taifa ya Serengeti unatokana na kuwa
na misururu mirefu ya nyumbu wanaohama kwa makundi na kuvuka hata mpaka
wa Tanzania hadi hifadhi ya wanyama pori ya Maasai Mara nchini Kenya ambapo
takwimu za TANAPA zinaonyesha kuwa kila mwaka zaidi ya nyumbu milioni
moja,pundamilia 200,000, swala tomi zaidi ya 300,000 na pofu 12,000 huunga
misafara ya kutafuta malisho na maji
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti huchukuliwa kama moja ya maajabu ya
dunia kutokana na tendo la uhamaji wa nyumbu kutoka kusini hadi kaskazini na
kurudi, tendo ambalo linafanyika mara moja tu kwa mwaka tendo hilo linaifanya
hifadhi hii kuwa Eden ya Afrika na kupendwa kutembelewa na watu wengi
ulimwenguni kote. Licha ya nyumbu wanyama wengine maarufu walao nyama katika
hifadhi ya Taifa ya Serengeti ni chui na samba, ambapo utafiti umebaini kuwa
ukubwa wa hifadhi hii umesaidia kudumisha uhai wa wanyama waliokuwa katika
hatari ya kutoweka kama vile faru weusi na duma
Watalii wanaotembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kutokana
na makundi makubwa ya nyumbu wameifanya hifadhi hiyo kuwa maarufu Afrika
mashariki na ulimwenguni kote hali iliyosababisha shirika la Umoja wa Mataifa
la Elimu na Sayansi UNESCO kuitangaza Serengeti kuwa eneo la urithi
wa Dunia kwa kuwa ndiyo eneo pekee ulimwenguni lililosalia kundi kubwa la
wanyama wahamao. Hifadhi ya Taifa ya
Serengeti ipo umbali wa kilometa 335 kutoka Arusha ikiambaa kaskazini katika
mpaka na nchi ya Kenya,kwa upande wa magharibi inapakana na na ziwa Viktoria.
Hifadhi hii inafikika kwa kukodi ndege kutokea jijini Dar es
salaam,Mwanza,Kilimanjaro na Arusha pia kwa barabara kutokea Arusha,Musoma na
Mwanza,wakati mzuri wa kutembelea hifadhi hii ili kuona uhamaji wa nyumbu ni
kuanzia mwezi Desemba hadi Julai.
Email: teresiamsanga@gmail.com
No comments:
Post a Comment